Uongozi

WAAJIRI BADILIKENI! Kutoa Ajira kwa Vigezo vya Taaluma na Uzoefu Pekee Kumepitwa na Wakati

🇬🇧 Read in English

Kiongozi na mfanyakazi wakizungumza kwa umakini na uwazi ofisini
Uongozi bora huanzia kwa kumsikiliza mtu kwa kweli — sio kuangalia vyeti pekee.

Katika miaka hii ni vigumu sana kukuta tangazo lolote la ajira ambalo haliweki mkazo wa kipekee kwenye vigezo vya kitaaluma na uzoefu wa kazi wa miaka kadhaa. Japokuwa huu ni utaratibu mwepesi wa kuchuja na kupata waombaji wa kazi, uchambuzi wa watu wengi wenye mafanikio, wa zamani na wa sasa, unaonyesha kuwa huenda utaratibu huu hauna ufanisi sana.

Nia ya mwajiri ni kupata mfanyakazi ambaye ataongeza thamani kwenye taasisi na kuyafanya malengo ya taasisi kufikiwa au hata kupitwa kwa wepesi zaidi. Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa vigezo vya taaluma na uzoefu wa miaka mara nyingi hawaongezi thamani ya kutosha kiasi cha kuifanya taasisi ifikie malengo na kung'ara.

Kwa upande mwingine, wafanyakazi walioajiriwa kwa sifa nyingine — hasa uwezo wa ushawishi na kuongoza, bila kujali viwango vyao vya taaluma na uzoefu kwenye kazi — huongeza thamani kubwa kwenye taasisi na kuifanya taasisi ing'are kwa mafanikio. Wafanyakazi hawa ni wale ambao wanatajwa kuwa na kiwango cha juu cha uwezo wa kutambua kwa uhakika na kushughulikia kwa namna bora hisia zilizomo ndani mwao na ndani ya watu wengine wenye mahusiano nao ya kikazi.

Emotional Intelligence Ni Nini?

Kitaalamu, uwezo huu hujulikana kama Emotional Intelligence (EI) au Emotional Quotient (EQ). Kuna miundo (models) miwili inayotumika kuutafsiri huu uwezo. Muundo wa kwanza ni ule uliopendekezwa na Konstantin Vasily Petrides mnamo mwaka 2001. Muundo huu, ambao kitaalamu huitwa trait model, unajumuisha mielekeo mbalimbali ya kitabia inayoonyeshwa na mtu, pamoja na uwezo na vipaji mhusika anavyojiona kuwa navyo.

Muundo wa pili ni ule uliopendekezwa na mabwana Peter Salovey na John Mayer mnamo mwaka 2004. Muundo huu, ambao kitaalamu huitwa ability model, huweka mkazo juu ya uwezo wa mtu kufanyia kazi taarifa zinazohusu maono/hisia za watu mbalimbali na jinsi ya kuzitumia taarifa hizo kwa weledi katika mazingira ya jamii aliyomo.

Tafiti Zinasema Nini

Tafiti zinaonyesha kuwa watu wenye EI kubwa huwa pia na kiwango cha juu cha ubora katika siha ya akili, wana utendaji kazi uliotukuka, na pia wana maarifa makubwa ya kuongoza. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Daniel Goleman na kuchapishwa katika kitabu chake kinachoitwa Working With Emotional Intelligence, EI inachangia kiasi cha 67% ya vigezo vyote vya lazima vinavyohitajika ili mtu aweze kuwa na utendaji uliotukuka katika uongozi. Aidha, kwa mujibu wa utafiti huu, umuhimu wa EI ulibainika kuwa mara mbili zaidi ukilinganisha na akili ya kiufundi (IQ) katika kuleta mafanikio ya kiuongozi.

Hadithi ya Charles Schwab

Hebu tuangalie mfano wa Bwana Charles Schwab katika kuthibitisha ukweli wa umuhimu wa EI katika uongozi. Huyu alizaliwa mwaka 1862 kule Williamsburg, Pennsylvania, na kufariki mwaka 1939. Charles Schwab hakumaliza elimu ya chuo. Baada ya kuhudhuria Chuo cha St. Fransis (sasa kinaitwa Chuo Kikuu cha St. Fransis) kwa miaka miwili, aliacha na kuelekea katika jiji la Pittsburgh kutafuta kazi.

Moja ya sifa kubwa za Charles Schwab ilikuwa ni uwezo mkubwa wa kushawishi. Kutokana na uwezo wake mkubwa, mwaka 1897 akiwa na miaka 35, alifanywa kuwa Rais wa kampuni ya kutengeneza chuma ya Carnegie Steel. Mwaka 1901 alisaidia kufanikisha majadiliano ya siri ya kuuzwa kwa kampuni hii, ambapo iliuzwa kwa kundi la wawekezaji kutoka New York waliokuwa chini ya J.P. Morgan. Kampuni hii ilibadilishwa jina na kuwa U.S. Steel Corporation, na Charles Schwab akawa Rais wake wa kwanza.

Hata hivyo, mwaka 1903 Charles Schwab aliondoka U.S. Steel baada ya kutoelewana na Morgan, na kujiunga na Bethlehem Shipbuilding and Steel Company. Chini ya uongozi wake, kampuni hii ilikua haraka haraka na kuwa ya pili kwa ukubwa duniani miongoni mwa makampuni ya chuma.

Kutokana na uwezo wake mkubwa, mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1920 Charles Schwab alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wanapata mishahara mikubwa ya kutisha. Kwa mujibu wa Dale Carnegie, mwandishi mashuhuri wa vitabu vya kufundisha mahusiano, wakati huo Charles Schwab alikuwa akipata mshahara wa dola za Kimarekani milioni 1 kwa mwaka — sawa na dola 2,740 kwa siku!

Pamoja na uwezo wa kushawishi, Charles Schwab alikuwa pia ni muumini wa kutoa motisha moja kwa moja kwa mtu aliyefanya vizuri, na siyo kuoanisha motisha ya mtu mmoja mmoja na utendaji wa kampuni. Imani hii ilifanya wafanyakazi wake wawe wabunifu na wenye kujitoa kwa hali na mali, kwa sababu watu walijua kuwa mwisho wa siku jitihada zao zitawalipa.

Waajiri wa Leo Wanaweza Kujifunza Nini

Bila shaka, waajiri wetu wa leo wana mengi wanayoweza kujifunza kutoka kwa Charles Schwab. Mafunzo watakayopata yatasaidia kugeuza maeneo mengi ya kazi kuwa maeneo yenye ufanisi zaidi!

🇬🇧 Read in English

Jiunge na mazungumzo