Je, Tunachoma Utambi?
Operesheni dhidi ya wafanyabiashara wadogo inaweza kuwa cheche inayowasha moto ambao hatutaweza kuuzima.
Jumamosi, tarehe 10 Oktoba 2026, niliona mambo mawili yaliyonitia hofu, na baadaye nikasimuliwa la tatu.
Lori la Takataka Lililobeba Watu
Jambo la kwanza lilikuwa lori kubwa la kusombea takataka likiwa limesheheni wafanyabiashara wadogo waliokamatwa pamoja na mali zao. Ndani ya lori hilo pia kulikuwa na kundi kubwa la wakamataji: vijana waliovaa sare rasmi za mgambo wa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa nini tukio hili liliniogopesha? Kwa sababu waliokamatwa ni vijana wasio na ajira rasmi, wanaopambana kujitafutia riziki kwa njia halali. Kuwazuia kufanya biashara ndogondogo zilizo ndani ya uwezo wao ni kuwatumia ujumbe hasi mno.
Ni sawa na kuwaambia: "Hamna haki ya kuishi!" Kinachotia hofu ni kwamba hakuna kiumbe kinachokubali kunyang'anywa uhai huku kikitazama tu.
Mtu Akinyimwa Riziki Halali
Katika kupigania uhai, binadamu hugeukia uhalifu. Hii iko katika asili yetu. Hata wezi na wala rushwa maofisini wako katika mapambano hayo hayo. Wameajiriwa kufanya kazi siku 30, lakini ujira wanaolipwa unatosha mahitaji ya siku 20 tu. Hesabu hii ndiyo jibu halisi la kwa nini rushwa na wizi vimeshamiri.
Kwa wale wasio na ajira rasmi, ambao pia wananyimwa haki ya kujitafutia riziki kwa njia halali, tutarajie ongezeko la vibaka na wakabaji mitaani. Huu utakuwa uhalifu wa aina ya kwanza.
Uhalifu wa aina ya pili, unaoogopesha zaidi, ni kuibuka kwa machafuko makubwa.
Machafuko makubwa kwa kawaida huishia kuchukua sura ya kisiasa. Yanahitaji nguvu kubwa mno kuyazima, na hata baada ya matumizi ya nguvu hiyo, mara nyingi serikali husika huishia kuanguka. Mifano ni mingi; hatuna haja ya kuitaja.
Bomoabomoa ya Mpanda: Je, ni Operesheni ya Nchi Nzima?
Nikiwa bado natafakari tukio hilo, likaibuka jingine. Rafiki yangu mmoja alinionyesha kipande cha video ya bomoabomoa iliyokuwa ikiendelea katika mji wa Mpanda, mkoani Katavi. Katika video hiyo, tingatinga la Halmashauri lilikuwa likivunja vibanda vya wafanyabiashara wadogo bila huruma.
Kwa nini tukio hili nalo liliniogopesha? Kwa sababu lilinijia wazo kwamba huenda "vita" dhidi ya wamachinga ni mradi unaolenga nchi nzima!
Hebu fikiria: vibaka na wakabaji wakiibuka nchi nzima. Utaacha kuogopa kweli?
Au jiulize: hatima ya machafuko yanayoweza kuibuka nchi nzima itakuwa ipi? Kama hilo halikuogopeshi, basi wewe si mtu wa kawaida!
Mbagala: Wachuuzi Wametoweka, Bei Zimepanda
Tukio la tatu ni simulizi ya rafiki yangu mwingine. Anaishi Buguruni, lakini kwa kawaida hununua mahitaji ya nyumbani, hasa vyakula, huko Mbagala. Anasema bei za vyakula Mbagala kwa ujumla ziko chini sana ukilinganisha na maeneo mengine ya jiji.
Aliniambia kuwa siku hiyo, kama kawaida yake, alikwenda Mbagala kununua mahitaji, lakini alikuta hali tofauti na aliyoizoea. Wachuuzi hawakuwepo; badala yake kulikuwa na mamia ya askari mgambo.
Baada ya kuulizauliza, alielekezwa vichochoroni ambako alipata alichohitaji, lakini kwa kificho na kwa bei ya juu kuliko aliyozoea.
Simulizi hii iliniongezea hofu. Soko kubwa la wakulima ni wafanyabiashara wadogo wa mijini. Kama wafanyabiashara hawa hawapo, wakulima hawana sababu ya kuleta mazao yao mjini.
Je, Kuna Mkono Usioonekana?
Rafiki yangu huyu anaamini kwamba ndani ya serikali kuna watu wanaotaka vurugu kubwa ziibuke nchini. Anaamini kuwa watu hao wanapokea "rushwa" kutoka mataifa ya nje na wanatumia kisingizio cha kuweka miji na majiji safi. Anasema hili limekuja baada ya kuona kwamba jaribio la kuzua vurugu kupitia ufadhili wa vyama vya siasa limeshindikana.
Sina uhakika na dhana hii ya pesa kutoka nje ya nchi kutumika kuchochea vurugu kupitia wafanyabiashara wadogo.
Ninachokiamini kwa uhakika ni kwamba kinachoendelea sasa kitazua matatizo huko tuendako.
Ombi kwa Mheshimiwa Rais
Siamini kuwa kinachoendelea kina baraka za Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia ni miongoni mwa marais bora kabisa kuwahi kutokea nchini. Tangu aingie madarakani amefanya mengi yenye lengo la kuboresha maisha ya Watanzania. Bila shaka anajua kuwa wananchi wake wengi hawana ajira rasmi, hivyo ni lazima wajitegemee katika kutafuta riziki. Si rahisi kwa kiongozi mwenye mtazamo huu kuagiza vitendo visivyo vya kiutu kama hivi vinavyoendelea.
Rais ana majukumu mengi sana, hivyo kuna mambo yanayoweza kufanyika bila yeye kujua.
Naomba sana, ikiwezekana, aweke utaratibu wa kukutana na wananchi uso kwa uso, angalau mara moja kwa mwezi, ili ajue kwa uhakika kinachoendelea. Hili halitakuwa jambo geni: Rais mwingine bora aliyewahi kutokea nchini, almarhum Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kufanya hivyo.
Wewe unaonaje? Je, tunachoma utambi? Toa maoni yako hapa chini, na mtumie makala hii mtu unayemjua.
Toa maoni yako