Ukuaji wa Biashara

Kwa Nini Biashara Nyingi Hufa Kabla ya Kufikisha Miaka 5 Tangu Kuanzishwa?

Takriban nusu ya biashara zote mpya hufungwa kabla ya kutimiza miaka mitano. Fahamu kwa nini hali hii hutokea, na hatua rahisi ya kulinda akiba yako na biashara yako.

🇬🇧 Read in English

Mwanamke akitabasamu nyuma ya kaunta ya duka lake dogo lililojaa bidhaa
Biashara ndogo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, lakini nusu yake hufungwa ndani ya miaka mitano. (Picha: Ali Mkumbwa / Unsplash)

Kila mwaka maelfu ya watu hufungua maduka, saluni, migahawa midogo, maduka ya vifaa vya ujenzi na biashara nyinginezo wakiwa na matumaini makubwa. Miaka michache baadaye, milango mingi ya biashara hizo imefungwa. Wamiliki wamepoteza akiba zao, wakati mwingine hata akiba za familia, na mara nyingi hawajui hasa ni nini kilichoharibika.

Kwa nini hali hii inatokea mara nyingi hivi? Na muhimu zaidi, ufanye nini ili biashara yako iwe bado imesimama siku inapotimiza miaka mitano?

Ni Biashara Ngapi Hasa Hufa Mapema?

Tafiti katika nchi zilizoendelea zinaonyesha kuwa biashara nyingi hufa kabla ya kusherehekea miaka 5 tangu kuzaliwa kwake. Takwimu za kuaminika zaidi za muda mrefu zinatoka kwa Ofisi ya Takwimu za Kazi ya Marekani (BLS), ambayo hufuatilia kila biashara mpya mwaka hadi mwaka:

Umri wa biasharaBiashara zinazoendelea kuwepo
Baada ya mwaka 1Takriban 80% (biashara 1 kati ya 5 imeshafungwa)
Baada ya miaka 5Takriban 50% (nusu zimefungwa)
Baada ya miaka 10Takriban 35% (karibu biashara 2 kati ya 3 zimefungwa)

Hii ni katika nchi ambayo ni rahisi sana kukopa, kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi na kupata wateja. Hapa Tanzania na sehemu kubwa ya Afrika Mashariki, ambako biashara ndogo zinakabiliwa na riba kubwa, ugumu wa kupata mikopo na sekta kubwa isiyo rasmi, hatari ya biashara kufa mapema inaweza kuwa kubwa zaidi.

Ukweli wa mambo ni kwamba hali hii inaogopesha: takriban nusu ya biashara zote mpya hazifikishi miaka mitano. Swali si kama hatari hii ipo, bali ni upande upi biashara yako itakuwepo.

Sababu 4 Kuu Zinazoua Biashara Changa

Tafiti, pamoja na uzoefu wangu wa kuwashauri wafanyabiashara wadogo hapa Dar es Salaam, zinaonyesha sababu zilezile chache.

1. Mtaji mdogo

Biashara nyingi huanzishwa kwa fedha zinazotosha kufungua mlango tu, bila kubaki na chochote cha kuuweka wazi. Kodi ya pango, bidhaa, leseni na mishahara lazima vilipwe muda mrefu kabla wateja hawajaanza kuja kwa wingi. Fedha zikiisha kabla mauzo hayajapanda, biashara hufa, hata kama wazo lilikuwa zuri.

2. Kushindwa kuajiri wafanyakazi wanaohitajika

Mmiliki anayelazimika kufanya kila kitu peke yake hukwama haraka. Bila watu wa kuuza, kuhudumia wateja, kutunza kumbukumbu za hesabu au kusimamia bidhaa, ubora hushuka, wateja huondoka na mmiliki huchoka kupita kiasi. Biashara nyingi ndogo hazipangi mapema wafanyakazi watakaohitajika wala jinsi ya kuwalipa.

3. Kiwango cha elimu na ujuzi wa msimamizi wa biashara

Kuwa hodari katika fani si sawa na kuwa hodari katika kuendesha biashara. Fundi cherehani, fundi magari au mpishi mwenye kipaji anaweza kuwa na uelewa mdogo kuhusu upangaji wa bei, utunzaji wa kumbukumbu, masoko au usimamizi wa fedha. Mapungufu haya hayaonekani siku ya kwanza, lakini hujitokeza ndani ya miaka miwili au mitatu.

4. Sababu zilizomchochea mmiliki kuanzisha biashara

Baadhi ya watu huanzisha biashara kwa sababu rafiki yao anafanya vizuri katika biashara kama hiyo, kwa sababu wamepoteza ajira na wanahitaji kitu cha haraka, au kwa sababu wamepata mafao na wanaona lazima "wafanye kitu". Biashara iliyoanzishwa bila kuwaelewa vizuri wateja wake, washindani wake na hesabu zake ni biashara iliyoanzishwa kwa matumaini tu.

Muuza nyama akiwa amesimama mlangoni pa duka lake dogo la nyama, samaki na kuku
Biashara zinazodumu ni zile ambazo wamiliki wake wanazijua hesabu zao. (Picha: Ali Mkumbwa / Unsplash)

Chanzo Kikuu: Kukosekana kwa Business Plan

Ukichunguza kwa makini, sababu zote nne zina chanzo kimoja. Kwa kifupi, biashara nyingi hufa mapema kwa sababu zimeanzishwa bila kuwepo mpango mahsusi wa biashara (Business Plan).

Business Plan kwa biashara ni kama ilivyo ramani kwa nyumba. Nyumba inayojengwa bila ramani itakuwa na makosa mengi, na uwezekano wa kudumu kwa muda mrefu ni mdogo. Kuta zinaweza kuwa mahali pasipo sahihi, paa lisitoshee, na jengo zima likaporomoka baada ya mvua kubwa za kwanza. Biashara iliyoanzishwa bila mpango ina udhaifu uleule. Inaweza kusimama kwa muda, lakini uwezekano wa kudumu ni mdogo.

Business Plan nzuri inakulazimisha kujibu maswali magumu kabla hujatumia fedha zako, si baada ya kuzitumia.

Maswali 7 Ambayo Business Plan Yako Lazima Ijibu

  1. Wateja wangu hasa ni akina nani, na kwa nini watanunua kwangu badala ya duka la jirani?
  2. Ninahitaji fedha kiasi gani hasa kufungua biashara, na kuiendesha kwa angalau miezi sita mauzo yakiwa chini?
  3. Nitarudisha gharama lini (break-even)? Ninahitaji mauzo kiasi gani kwa siku au kwa mwezi ili kulipa gharama zote?
  4. Nitauza kwa bei gani, na je, bei hiyo inaacha faida halisi baada ya kulipa kila gharama?
  5. Nitahitaji kuajiri nani, lini, na nitawalipa vipi?
  6. Ni ujuzi gani ninaoukosa, na nitaupataje au nitampata nani mwenye ujuzi huo?
  7. Nitafanya nini mambo yakienda vibaya? Msimu wa mauzo hafifu, mshindani mpya, au wasambazaji kupandisha bei.

Kama huwezi kujibu maswali haya kwa maandishi, bado hujawa tayari kuwekeza. Kama unaweza, tayari umeondoa sehemu kubwa ya sababu zinazoua biashara changa. Pia utakuwa na nyaraka ambazo benki, wawekezaji na wabia wataomba kuziona pale utakapohitaji mtaji zaidi.

Tayari Una Biashara? Angalia Dalili Hizi za Hatari

  • Hujui, bila kubahatisha, kama ulipata faida mwezi uliopita.
  • Fedha za biashara na fedha za nyumbani zinatoka mfuko mmoja.
  • Mara kwa mara unakopa ili kununua mzigo au kulipa kodi ya pango.
  • Mauzo yanategemea wewe kuwepo dukani kila siku.
  • Huna mpango wa maandishi wa miezi 12 ijayo.

Kama dalili mbili au zaidi zinakuhusu, bado hujachelewa. Kuandika Business Plan sasa, hata kwa biashara inayoendelea tayari, ni moja ya njia za gharama nafuu kabisa za kulinda ulichokijenga.

📘 Andika Business Plan Yako kwa Usahihi

Jalada la Andika Business Plan Inayoaminika na Benki na Wawekezaji, na Juma Killaghai

Kifurushi Andika Business Plan Inayoaminika na Benki na Wawekezaji kinakuongoza hatua kwa hatua katika kila sehemu ya business plan, kwa mfano halisi wa Kitanzania.

Ndani yake: mwongozo wa kurasa 55, violezo 8 vya Word vilivyo tayari kutumika na Excel Financial Planner inayokokotoa gharama za kuanzia, kiwango cha kurudisha gharama (break-even), mtiririko wa fedha na faida.

Jinsi ya kukipata:

  1. Bofya kiungo cha Payhip
  2. Bonyeza "Buy Now" na ukamilishe malipo
  3. Pakua mwongozo, violezo na Excel planner papo hapo

Gharama ni dola 15 tu, kidogo sana ukilinganisha na hasara ya uamuzi mmoja mbaya wa kibiashara.

👉 Pata kifurushi cha Business Plan

Unapendelea Kiingereza? Pata toleo la Kiingereza

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara

Ni asilimia ngapi ya biashara hufa ndani ya miaka 5?

Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu za Kazi ya Marekani (BLS), takriban 20% ya biashara mpya hufungwa katika mwaka wa kwanza, na takriban nusu hufungwa ndani ya miaka mitano. Baada ya miaka kumi, karibu biashara 2 kati ya 3 zimeshafungwa.

Sababu kubwa ya biashara ndogo kufa ni ipi?

Sababu zinazojitokeza zaidi ni mtaji mdogo, kushindwa kuajiri watu sahihi, mapungufu ya ujuzi wa mmiliki katika kuendesha biashara, na kuanzisha biashara kwa sababu zisizo sahihi. Nyingi kati ya hizi zinatokana na kuanzisha biashara bila business plan.

Je, business plan inasaidia kweli biashara kudumu?

Ndiyo. Business plan inakulazimisha kuchambua wateja, gharama, kiwango cha kurudisha gharama, wafanyakazi na hatari kabla hujawekeza, hivyo inaondoa sababu nyingi zinazoua biashara changa. Pia ndiyo nyaraka ambayo benki na wawekezaji huiomba.

Je, nimechelewa kuandika business plan kama biashara yangu tayari inaendelea?

Hapana. Mpango unaoandikwa kwa biashara inayoendelea hukusaidia kuona wapi fedha zinapotea, kuweka malengo ya miezi 12 ijayo na kujiandaa kwa mkopo au uwekezaji mpya.

Neno la Mwisho

Nusu ya biashara zote mpya hufungwa kabla ya kutimiza miaka mitano. Nyingi kati ya hizo hazifi kwa sababu mmiliki alikuwa mvivu au wazo lilikuwa baya. Zinakufa kwa sababu zilijengwa bila ramani. Kama unafikiria kuanzisha biashara, zingatia sana jambo hili: jenga biashara yako kwenye karatasi kwanza.

Ungependa kuandaliwa Business Plan? Wellbiz Solutions huandaa business plan, nyaraka za mikopo na maandiko ya miradi (proposals). Piga simu au WhatsApp: +255 754 281 131 / +255 655 281 131

Unamfahamu mtu anayetaka kuanzisha biashara? Mshirikishe makala hii kwanza.

Vyanzo: Ofisi ya Takwimu za Kazi ya Marekani (US Bureau of Labor Statistics), takwimu za kudumu kwa biashara, kama zilivyofupishwa na SCORE, "Small Business Failure Rates in 2024"; CB Insights. Makala asili ya Kiswahili na Juma Killaghai.

🇬🇧 Read in English

Toa maoni yako