Mtazamo wa Biashara

Jifunze Jambo Kubwa Sana Toka kwa Jack Ma! Kushindwa ni Kawaida, Kukata Tamaa Ndiko Kifo cha Maendeleo (Hatua 7 za Kujifunza Kutokana na Kushindwa)

Alikataliwa kazi takriban 30, akakataliwa na KFC, polisi na Harvard mara kumi. Muasisi wa Alibaba anatuonyesha kwamba "hapana" si mwisho wa safari.

🇬🇧 Read in English

Kujifunza kutokana na kushindwa: wapanda mlima wakipanda Mlima Kilimanjaro hatua kwa hatua
Hakuna anayefika kileleni mwa Kilimanjaro kwa hatua moja. Mafanikio hupandwa vivyo hivyo. (Picha: Crispin Jones / Unsplash)

Wengi wetu tumewahi kukataliwa: barua ya kuomba kazi isiyojibiwa, mkopo uliokataliwa, biashara iliyofungwa. Ni rahisi kufikia hitimisho kwamba sisi hatukuandikiwa kufanikiwa. Hadithi ya Jack Ma, muasisi wa kampuni ya Alibaba, inasema vinginevyo. Ni mojawapo ya mafunzo bora kabisa ya kujifunza kutokana na kushindwa, na inaanza na orodha ndefu ya neno "hapana".

Kwa Maneno ya Jack Ma Mwenyewe: Orodha Ndefu ya Kukataliwa

Jack Ma amesimulia hadithi hii kwenye mahojiano na hotuba nyingi, ikiwemo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya, mwaka 2017. Kwa maelezo yake mwenyewe:

"Nilifanya mtihani wa kujiunga na chuo kikuu mara tatu ndipo nikapata nafasi. Nilituma maombi ya kazi takriban mara 30, na mara zote nilikataliwa. Mgahawa wa KFC ulipokuja mjini kwetu, tuliomba watu 24; 23 waliajiriwa, ni mimi peke yangu niliyekataliwa. Tuliomba kujiunga na jeshi la polisi watu watano; wanne walikubaliwa, na kwa mara nyingine ni mimi peke yangu niliyekataliwa. Niliomba kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani mara 10, na mara zote walinikataa."

Huyo ndiye mtu ambaye, mwaka 1999, aliwakusanya marafiki 18 kwenye nyumba yake ndogo mjini Hangzhou na kuanzisha Alibaba. Miaka kumi na tano baadaye, mwaka 2014, Alibaba iliingia Soko la Hisa la New York na kukusanya takriban dola za Kimarekani bilioni 25, uuzaji mkubwa zaidi wa hisa duniani kwa wakati huo.

Alipo leo: Jarida la Forbes lilikadiria utajiri wa Jack Ma kuwa takriban dola za Kimarekani bilioni 25.4 tarehe 29 Oktoba 2026, akiwa karibu nafasi ya 95 duniani. Hata akiwa kileleni, changamoto hazikukoma: utajiri wake ulizidi dola bilioni 60 mwaka 2020, kisha ukashuka sana baada ya mamlaka kusimamisha mpango wa kampuni yake ya malipo, Ant Group, kuingia soko la hisa.

Tunajifunza Nini?

Hata siku moja usikate tamaa kwa sababu umeshindwa mara moja, mbili, na kadhalika. Kushindwa wakati mwingine ni mpango wa Mungu ili kukutanabahisha kwamba mafanikio yako yatapatikana kwenye mambo mengine tofauti na hayo unayojaribu kufanya. Jack Ma hakuandikiwa kukaanga kuku KFC (kampuni ambayo, kwa njia, Colonel Sanders alianza kuisambaza kwa mfumo wa franchise akiwa na miaka sitini na kitu) wala kuvaa sare ya polisi. Aliandikiwa kujenga kitu ambacho kilikuwa bado hakijawepo.

Kushindwa ni jambo la kawaida. Kushindwa ni sehemu ya kujifunza. Tatizo ni kukata tamaa, kwani kukata tamaa ni tangazo la kifo cha maendeleo yako! Kama Jack Ma alivyowaambia wanafunzi wa Nairobi: "Lazima uzoee kushindwa."

Kwa Nini Kushindwa Kunauma Sana (na Kwa Nini Kusikuzuie)

Kushindwa kunauma kwa sababu tunakuchukulia kibinafsi. Barua ya kukataliwa inaonekana kama hukumu juu ya sisi ni nani, wakati kwa kweli ni matokeo ya jaribio moja tu, kwa wakati mmoja, kwa njia moja. Ukitenganisha tukio na utu wako, kushindwa kunageuka kuwa taarifa badala ya hukumu.

Wafanyabiashara wanalijua hili kuliko mtu yeyote. Biashara nyingi hufungwa katika miaka yake ya mwanzo, na wafanyabiashara wengi waliofanikiwa walifunga biashara moja au mbili kabla ya kuipata ile iliyofanya kazi. Tofauti kati ya wanaofanikiwa mwishowe na wasiofanikiwa mara chache huwa kipaji. Ni kile wanachofanya baada ya kushindwa.

Mjasiriamali kijana akipitia mpango wake kwenye kompyuta baada ya kushindwa
Kila anguko lina somo ndani yake. Washindi ni wale wanaolichunguza. (Picha: Collins Lesulie / Unsplash)

Hatua 7 za Kujifunza Kutokana na Kushindwa na Kuinuka Tena

  1. Jipe muda mfupi wa kuumia, kisha simama. Kusikitika ni jambo la kawaida. Jipe siku moja au mbili, kisha elekeza akili yako kwenye mafunzo.
  2. Tenganisha tukio na utu wako. Sema "duka langu limeshindwa", si "mimi ni mtu wa kushindwa". La kwanza linarekebishika; la pili linakumaliza nguvu tu.
  3. Andika tathmini ya ukweli. Kwenye ukurasa mmoja jibu: nilipanga nini, kilichotokea ni nini, kwa nini kilitokea, na nitafanya nini tofauti?
  4. Hesabu kila "hapana" kama taarifa. Wateja kumi wakisema bei yako iko juu, huo ni utafiti wa soko umeupata bure. Tafuta mwenendo unaojirudia.
  5. Baki na lengo, badilisha njia. Jack Ma hakuacha kutaka kujenga kitu; aliendelea kubadilisha njia. Badilisha bidhaa, eneo, wateja au mbinu, si ndoto yako.
  6. Jaribio lijalo, shindwa kidogo na kwa gharama ndogo. Jaribu wazo jipya kwa mzigo mdogo, wiki moja ya majaribio au wateja wachache kabla ya kuwekeza akiba yako.
  7. Weka tarehe ya jaribio lijalo na mwambie mtu. Tarehe ya mwisho na mtu atakayekuuliza vinageuza nia kuwa vitendo.

Mfano halisi: genge la pili la juisi la Asha

Asha alifungua genge la juisi karibu na jengo la ofisi lenye watu wengi jijini Dar es Salaam, akalifunga baada ya miezi minne. Badala ya kusema "biashara si yangu", aliandika tathmini yake: bei zake zilikuwa sawa, lakini alikuwa akifungua saa 4 asubuhi wakati wateja wengi walitaka kifungua kinywa saa 1 asubuhi, na hakuwa na namba ya kupokea malipo kwa simu. Alifungua tena kwa bajeti ndogo zaidi, saa 12:30 alfajiri, akiwa na namba ya malipo ya simu mezani na ofa ya kifungua kinywa ya juisi na kitafunwa. Ndani ya miezi miwili mauzo yake ya kila siku yalikuwa juu sana kuliko jaribio la kwanza. Mtu yuleyule, lengo lilelile, njia tofauti. (Mfano wa kufundishia.)

SwaliJibu la Asha
Nilipanga nini?Kuuza vikombe 80 kwa siku kwa wafanyakazi wa ofisi.
Kilichotokea ni nini?Takriban vikombe 30 kwa siku; wateja wengi walikuja kabla ya saa 3 asubuhi.
Kwa nini?Muda mbaya wa kufungua; hakuna malipo kwa simu.
Nitabadilisha nini?Kufungua saa 12:30 alfajiri, kuongeza malipo kwa simu na ofa ya kifungua kinywa.

⚠️ Kutokata tamaa si ukaidi. Kutojikatia tamaa hakumaanishi kuendelea kumwaga akiba kwenye biashara inayoendelea kupata hasara. Kama hesabu zinabaki nyekundu hata baada ya kurekebisha matatizo yaliyo wazi, badilisha mwelekeo. Soma makala yetu ya kwa nini biashara nyingi hufa kabla ya miaka 5 ili kuziona dalili za hatari mapema.

📘 Unaanza Upya? Hujachelewa: Mwongozo + Zana 10

Iwe una biashara iliyoshindwa nyuma yako au unadhani umri umekupita kujaribu tena, kifurushi hiki cha vitendo kinakusaidia kuanzisha (au kuanzisha upya) biashara bila kuhatarisha akiba yako:

  • Mwongozo wenye picha wa kurasa 30: hatua 10 kuanzia kutambua ulichonacho hadi mpango wa uzinduzi wa siku 90
  • Mpango wa siku 30 wa "Jaribu Kabla ya Kuwekeza", ili jaribio lako lijalo, likishindwa, lishindwe kidogo
  • Mpango wa Kulinda Akiba (Kanuni ya Mafungu Matatu), Kipimo cha Mawazo ya Biashara na mpango wa biashara wa ukurasa mmoja (Word)
  • Kikokotoo cha Excel cha gharama za kuanzia, bei na break-even

👉 Pata Hujachelewa ($15)

Toleo la Kiingereza: Never Too Late. Unahitaji msaada wa kuchambua kilichoharibika na kupanga jaribio lako lijalo? Piga simu au WhatsApp +255 754 281 131 / +255 655 281 131

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara

Je, ni kweli Jack Ma alikataliwa kazi na KFC?

Ndiyo, kwa maelezo yake mwenyewe. Jack Ma amesimulia mara nyingi, ikiwemo kwenye hotuba yake katika Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 2017, kwamba KFC ilipofika mjini kwao waliomba kazi watu 24 na 23 wakaajiriwa. Yeye peke yake ndiye aliyekataliwa. Anasema pia aliomba kazi takriban 30, alikataliwa na polisi, na Harvard ilimkataa mara 10.

Nitajifunzaje kutokana na kushindwa badala ya kukata tamaa?

Tenganisha tukio na utu wako, andika tathmini fupi ya ukweli kuhusu kilichotokea na sababu zake, baki na kilichofanya kazi, badilisha jambo moja au mawili, jaribu njia mpya kwa gharama ndogo, na weka tarehe ya jaribio lako lijalo. Kushindwa kunafundisha pale tu unapokuchunguza.

Ni wakati gani niache kujaribu na kubadili mwelekeo?

Baki na lengo lakini uwe tayari kubadili njia. Kama hesabu zinaonyesha biashara inaendelea kupata hasara hata baada ya kurekebisha matatizo yaliyo wazi, acha kumwaga akiba yako humo na elekeza nguvu mahali pengine. Kutokata tamaa maana yake ni kutokujikatia tamaa wewe mwenyewe, si kukataa kubadilika.

Utajiri wa Jack Ma ni kiasi gani leo?

Jarida la Forbes lilikadiria utajiri wa Jack Ma kuwa takriban dola za Kimarekani bilioni 25.4 tarehe 29 Oktoba 2026, akiwa karibu nafasi ya 95 duniani. Utajiri wake ulizidi dola bilioni 60 mwaka 2020 na kushuka sana baada ya mamlaka kusimamisha mpango wa kampuni yake ya Ant Group kuingia soko la hisa.

Neno la Mwisho

Jack Ma alisikia neno "hapana" mara nyingi kuliko wengi wetu tutakavyowahi kulisikia. Kila kukataliwa kulimsogeza karibu kidogo na njia iliyokuwa yake kweli. Kushindwa ni jambo la kawaida. Kushindwa ni sehemu ya kujifunza. Kukata tamaa ndilo jambo pekee linaloua maendeleo yako. Chunguza anguko lako, badilisha njia, na piga hatua inayofuata kupanda mlima.

Unahitaji msaada? Wellbiz Solutions huwasaidia wajasiriamali kuchambua biashara zao, kuandika mipango ya biashara inayotekelezeka, na kusajili na kuanza upya kwa kujiamini. Piga simu au WhatsApp: +255 754 281 131 / +255 655 281 131

Unamfahamu mtu anayekaribia kukata tamaa baada ya kuanguka? Mtumie makala hii.

Vyanzo: Forbes, wasifu wa Jack Ma wa utajiri wa papo hapo (ulitazamwa 29 Oktoba 2026); CNBC, "The lesson Alibaba's Jack Ma learned after being rejected for a job at KFC" (9 Agosti 2017, kuhusu hotuba yake Chuo Kikuu cha Nairobi); mahojiano na hotuba za Jack Ma mwenyewe. Makala asili imeandikwa na Juma Killaghai.

🇬🇧 Read in English

Changia maoni yako